Thursday, December 3, 2009

TRL HAKUKALIKI.......................!!!!!


JESHI la Polisi jana lilimnusuru mkurugenzi wa Kampuni ya Reli nchini (TRL), Hundi Chaudhary na menejimenti yake baada ya wafanyakazi kutaka kuwaondoa ofisini kwa nguvu.

Pamoja na kushindikana kwa jaribio hilo, wafanyakazi wa TRL wameamuru treni ya abiria, ambayo imetoka Dar es salaam juzi kuelekea mikoa ya Kanda ya Ziwa, isiendelee na safari mara itakapofika Itigi ambako wametaka abiria wote washushwe.

Hasira za wafanyakazi hao, ambao wamekuwa wakimpinga kwa nguvu zote mwekezaji kwenye kampuni hiyo kubwa ya usafiri nchini, zimeongezeka kutokana na kutolipwa mishahara yao ya mwezi Novemba na hasa baada ya menejimenti kuwaambia kuwa haina fedha za kuwalipa mishahara.

Jaribio la kumwondoa mkurugenzi huyo lilifanywa baada ya wafanyakazi kufanikiwa kumwondoa msimamizi wa karakana ya kampuni hiyo iliyo Dar es salaam na kumtaka asionekana tena ofisini.

Kamanda wa poli kitengo cha Reli, Ruth Makelemo alisema baada ya tukio hilo kuwa wafanyakazi hao na uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU) hawana mamlaka ya kuifukuza menejimenti ya TRL nchini.

Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya mkurugenzi huyo wa TRL, Chaudhary jijini Dar es Salaam.

“Mimi siwezi kuruhusu wafanyakazi kuwaondoa hawa jamaa ofisini kwa sababu hawana kibali cha kufanya hivyo. Nitawalinda mpaka dakika za mwisho pamoja na mali zao,” alisema Makalemo.

"Hali si shwari hapo nje wafanyakazi wamefunga barabara; hakuna hata pa kupita, je nikiruhusu waondoke kisha ikatokea mauaji hapo nje, nitajibu nini mbele ya viongozi wangu; wakitaka walete kibali kwanza vinginevyo hapa hatoki mtu.”

Msimamo wa ofisa huyo wa polisi ulizidisha hasira za wafanyakazi hao ambao baadaye walilazimika kugoma kufanya kazi na kusitisha huduma zote za treni hiyo hadi watakapopata mishahara yao.

“Kwa kuwa polisi mmeamua kutuzuia kumwondoa mwekezaji, sisi tunasitisha huduma zote za reli mpaka hapo tutakapolipwa haki yetu na pia hatutarudi kazini mpaka Wahindi waondoke,” alisema mmoja wa wafanyakazi aliyekuwa mstari wa mbele.

Baadaye wafanyakazi hao waliwaamuru wafanyakazi wa kitengo cha kuongoza safari za treni kupiga simu kwenye vituo vyote vya reli ili waizuie treli ya abiria iliyokuwa imeondoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya bara jana.

Na kiongozi huyo wa kitengo cha safari za treni ambaye jina lake halikufahamika mara moja alisikika akizungumza kwa simu akisema: “Hapa Dar es Salaam hali si shwari. Wafanyakazi wameamuru treni ya abiria ikifika Itigi isimame na isiendelee na safari zake mpaka hapo itakapo tangazwa tena.”

Treni hiyo ya abiria iliondoka Dodoma jana saa 2:30 asubuhi kuelekea mikoa ya Mwanza, Tabora, Kigoma na Shinyanga lakini mpaka taarifa hiyo inatolewa jana mchana ilikuwa imefika Manyoni, lakini wakataka ishushe abiri Itigi.

Mkurugenzi mkuu wa TRL, Hundi Chaudhary hakutaka kuzungumzia lolote kuhusu jaribio hilo la wafanyakazi.

“Jamani ningependa mnipe nafasi kidogo nipumzike. Kichwa changu kimechoka sana; siwezi kuzungumza chochote leo,” alisema Chaudhary.

Katibu mkuu wa TRAWU Sylvester Rwegasira alisema chama chake hakikushiriki kumwondoa mwekezaji huyo na badala yake kilikuwa kinafanya naye mazungumzo ili aondoke mapema kabla ya jazba za wafanyakazi hao hazijakithiri.

TRL ni kampuni iliyoundwa kwa ubia baina ya serikali na kampuni ya Rites ya India, ambayo ilishinda zabuni ya kuendesha huduma hiyo nyeti ya usafiri wa reli nchini. Rites imesaini mkataba wa miaka 25 na serikali, ambayo hata hivyo inaonekana kusita kuvunja mkataba ikidai italazimika kulipa fidia kubwa.

Mkataba wa serikali na Rites, ambayo inamiliki asilimia 51 ya hisa, ulisainiwa Oktoba mosi Mwaka 2007.

No comments:

Post a Comment